Wamekula ya Mbuzi ...Wanaota Mapembe

Migogoro mingi katika bara la Afrika hutokea kwa sababu ya Madaraka, Viongozi wengi wanapotaka kuingia madarakani hutoa ahadi zenye kuvutia kwa wananchi wao lakini mara wanapoingia madarakani utamu wa madaraka huwazidi na kujikuta wakijaribu kadri wawezavyo kubadilisha Katiba ili waendelee kuongoza. Hali ambayo huzusha migogoro. Ama kweli "Wamekula ya Mbuzi sasa Wanaota Mapembe".

Friday, October 21, 2005

'PCB imekumbuka blanketi kukiwa kumekucha'



HIVI karibuni Taasisi ya Kuzuia Rushwa Tanzania (PCB), iliendesha kongamano katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam, lililokuwa na lengo la kuweka mikakati ya kukabiliana na rushwa katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Pamoja na mambo mengine kongamano hilo lilikuwa na lengo la kuhakikisha kuwa PCB inapambana vilivyo na vitendo vya rushwa ambavyo vinaweza kujitokeza katika uchaguzi huo, ambao ni muhimu na nyeti nchini katika kujipatia viongozi ambao wamechaguliwa kihalali.

Ni kweli, kongamano hilo lilikuwa muhimu sana kwani yawezekana mikakati yake na utekelezaji utakaochukuliwa baada ya hapa, utabadilisha kabisa mipango ya baadhi ya wagombea kupanga kutoa rushwa kama njia ya kuungwa mkono na hivyo kuchaguliwa.

Katika hili kuna kila sababu ya kuipongeza taasisi hii muhimu sana katika kampeni zake za kupambana na mdudu rushwa ambaye kwa kweli ametanda na kuota mizizi katika kila sehemu ya nchi yetu, na matokeo yake kuzidi kuwatafuna wananchi wa tabaka la chini ambao ndio wengi zaidi hapa nchini.

Kutafunwa huko kwa 'walalahoi', kumekuwa kukiwakosesha Watanzania hao haki muhimu zaidi kwao kama vile katika kupewa huduma za kijamii zikiwemo matibabu, elimu, maji na nyinginezo.

PCB imewahi kutafiti mambo mbalimbali ya kijamii kama pale ilipoweza kuzunguka nchi nzima na kusikiliza kero za wafanyakazi hususani walimu, na kubaini kwamba baadhi walikuwa wakikosa mishahara yao kutokana na baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya nchini 'kuitafuna'.

Hatua hiyo ilipokelewa kwa uzito na mvuto wa aina yake kwa Watanzania kwani pamoja na matokeo mengine lakini pia lilisababisha kusimamishwa kazi kwa karibu Wakurugenzi 15 wa halmashauri zilizohusika na ubadhilifu wa fedha za mishahara ya walimu na watendaji mbalimbali katika halmashauri zao.

Mpaka sasa bila shaka kuna kesi za watuhumiwa hao zikiwa zinaendelea kusikilizwa katika Mahakama mbalimbali baada ya kufikishwa mahakamani mara tu baada ya kusimamishwa kazi.

Pamoja na mambo mengi mazuri ambayo yamefanywa na taasisi hiyo katika kampeni zake za kupambana na rushwa nchini, katika hili la kuitisha kongamano kuzungumzia rushwa kwenye uchaguzi, mimi naona kuwa wamechelewa mno kuweka mikakati yao ya kupambana na rushwa.


Nalazimika kupingana na PCB, kwa vile mikakati ya kupambana na rushwa iliyojadiliwa karibuni, haikufaa kujadiliwa karibu wiki tatu kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika. Hili si sahihi kabisa.

Nasema hivyo nikiamini kwamba wakati wa uchaguzi, baadaye mwezi huu, sidhani kama kuna mgombea ambaye ataweza kutoa rushwa kwa wapiga kura wake, kwani ni vigumu mno kutoa rushwa kwa wapiga kura maelfu ambao watapiga kura siku hiyo.

Mikakati kama hiyo ingefanyika wakati wa maandalizi ya kuwapata wagombea katika nafasi mbalimbali, michakato ambayo ilikuwa inafanywa na watu wachache wakiwawakilisha wengine kupitia vyama vyao.

Katika michakato hiyo hasa tukiangalia katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), kulikuwa na wagombea mbambali ambao walikuwa wanajitokeza na kuchukua fomu kisha kuanza kampeni ya kura za maoni hatimaye kujikusanya kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya mkutano ambao ulikuwa una jukumu la kumchagua mgombea ubunge kupitia upigaji kura.

Hatua hii nadhani ndiyo iliyohusisha rushwa za kila aina ambayo nadiriki kusema haitatokea wakati mwingine wowote katika uchaguzi wa mwaka huu. Wagombea hawa walikuwa wakihakikisha kuwa wanakutana na karibu wajumbe wote wa kura za maoni kutoka katika jimbo zima ili kuwashawishi.

Kwa mazingira kama haya, mgombea alikuwa na uwezo wa kutoa rushwa kwa wapigaji kura wote au hata zaidi ya nusu ambao ana uhakika kuwa wangeweza kumpatia ushindi katika kura hizo za maoni.

Ni katika kipindi hicho ndipo ilihitajika mikakati kama hiyo ya PCB ambayo wameiweka sasa, kwani ni katika kipindi hicho pia rushwa ilipunguzwa makali na kuhararishwa kwa kupewa jina la 'Takrima', na hivyo kuwapa nafasi baadhi ya wagombea kutoa rushwa hadharani na kudai kuwa ni takrima na si rushwa.

Si lengo langu kuwapinga PCB katika mikakati yao, bali hapa nataka kusema kuwa 'PCB wamekumbuka shuka wakati kumekucha', hii ni kweli kabisa kuwa katika uchaguzi mkuu ujao ambao utawashirikisha wananchi wote nchini wenye sifa ya kupiga kura hautakuwa na rushwa kama ilivyokuwa katika kura za maoni.

Ni vigumu zaidi kutoa hongo kwa wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura katika jimbo zima tofauti ilivyokuwa kwenye kura za maoni ambapo wajumbe wachache tu ndio walikuwa wanapiga kura.

Hii inaleta mashaka kama ni kweli mikakati hiyo imelenga kuondoa rushwa katika uchaguzi huo kwani kwenye mchakato wa kura za maoni ndiko kulikuwa na kila aina ya rushwa ambazo zilikuwa zinatolewa.

Pia hapa lazima kuwe na shaka kuwa kwa nini taasisi hiyo ilikaa kimya katika mchakato huo na sasa kuamka na kuanza kuweka mikakati kwenye sehemu ambayo hatuna uhakika kama kutakuwa na vitendo kama vilivyofanyika wakati huo.

Katika hili inadhihirisha kuwa taasisi hiyo haiko huru kufanya mambo yake. Kura za maoni zilipambwa na Takrima kama ilivyoitwa na ilifikia kipindi baadhi ya wanachama wa CCM walitamka hadharani kuwa walitumia Takrima katika kupita kwenye kura za maoni.

Pamoja na kusema hivyo PCB haikutoa tamko lolote juu ya ufuatiliaji wa mambo hayo, hali iliyofikia baadhi ya wanachama wa vyama hivyo kuiomba taasisi hiyo kuanzisha uchunguzi juu ya matukio hayo.

Ninachopenda kusema ni kuwa taasisi hiyo inapaswa kufanya kazi yake kwa kuendana na matukio yaliyoko katika wakati husika ili kupambana zaidi na vitendo ambavyo vinawakosesha haki wananchi wa kawaida hasa katika mchakato mzima wa uchaguzi kama huu.

Ushahidi mzuri katika hili, unapatikana kwa wananchi wenyewe ambao sasa wameamua kuachana na ile hali ya ndio mzee, hali ambayo mwananchi alikuwa anakubaliana na kila linalosemwa na kiongozi wake.

Wananchi hawa katika kuonesha kukerwa kwao na vitendo hivyo wamekuwa wakiwazomea wagombea waliopatikana kwa njia hizo tena mbele ya wagombea wa ngazi ya urais na kudai kuwa hawawataki.

Hili ni fundisho kwao kutoka kwa wananchi na machungu ambayo wanaanza kuyapata wagombea hao waliotumia nguvu ya mali katika kushinda kura za maoni.

Hapa taasisi ijaribu kuangalia na kuchunguza kwenye maeneo ambayo wagombea hao walizomewa kujua je wagombea hao walipatikana kihalali au la!, ili kuondoa wasiwasi ambao umeanza kutanda juu ya utendaji wa PCB.

Kwa kufanya hivyo kutarudisha imani ya watanzania kwenye taasisi hiyo na itadhihirisha kuwa inafanya kazi kwa uhuru na kuondoa dhana kuwa rushwa ni ile inayotolewa na wananchi wa kawaida wakati viongozi wao hutoa Takrima na si rushwa.

ends

7 Comments:

Post a Comment

<< Home