"Kupanga ni Kuchagua"

Kila mwanadamu ana mamlaka ya kubadilisha maisha yake kwa kutumia mazingira aliyo nayo! Mipango mibovu ya maisha yake husababisha maisha yake kuwa mabovu na Mipango bora ya maisha yake husababisha maisha yake kuwa Bora. Hivyo basi chagua maisha yako unataka yaweje?

Wednesday, March 16, 2005

HIVI UKABILA UNA NAFASI KATIKA MBIO ZA KUMTAFUTA RAIS MWAKA HUU?

Ni swali gumu sana katika uwezo wa kichwa changu kuweza kulipatia jibu sahihi ambalo kila mtu au walio wengi wanaweza kukubaliana nalo au kulirekebisha kiurahisi na kuleta maana halisi niliyokusudia.

Si swali ambalo mtu mwingine anaweza kujiuliza labda linatokana na mahesabu ya kutumia kikokotozi au ni mahesabu ya kimetriki La hasha! Ni swali ambalo linatakiwa utumie busara na akili zako za kuzaliwa ili uweze kulijibu.

Kwa upande mwingine hujaribu kulifananisha swali hili na mchezo wa karata tatu, ikimaanisha mchezo wa pata potea au kitendawili ambacho jibu lake ni gumu lazima upewe mji ili uweze kukiteguwa, hiyo ilikuwa enzi zetu za miaka ile tulipokuwa tunatengeneza magari kwa kutumia udongo au mabua ya mahindi.

Kihistoria nchi yetu imepitia katika vipindi vitatu tofauti vya uongozi, ambapo viongozi watatu tofauti waliongoza nchi yetu kufikia hapa tulipo huku tukitizamia ni nani atakuja kurithi jahazi hili katika kuipindi cha nne baadae mwaka huu,

Katika vipindi hivyo ambavyo kwa njia moja ama nyingine vilikuwa ni vipindi vya mpito ambavyo, vilihitaji viongozi wenye msimamo ukiwa hasa wa kujenga umoja na utaifa usiozingatia rangi, kabila au itikadi ya kidini, hali ambayo kwa njia moja ama nyingine naweza kusema kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliifanikisha kazi hiyo kiuthabiti kabisa!.

Baada ya kujenga misingi imara ya umoja wa taifa letu na wananchi kujiona kama ni watoto wa familia moja ikimaanisha kuwa wote ni watanzania pasipo kujali tofauti zao Mwalimu Nyerere alimtupia kazi ya kuliongoza jahazi la nchi yetu kwa kiongozi mwingine maarufu ndugu Alhaji AlHassani Mwinyi.

Kwa kuwa tayari misingi mizuri ya umoja wa taifa ilikuwa imejengwa na mwalimu kazi moja tu aliyokuwa nayo Ndugu Mwinyi ilikuwa ni kuhakikisha kuwa mipango yote iliyoachwa na Mwalimu inakamilishwa na kuanzisha mipango mingine yeynye lengo la kuendeleza nchi yetu.

Hakuna ambaye anaweza kupinga hili kuwa katika enzi za uongozi wa Mwinyi, alifunguwa milango ya kila kitu ambacho kilikuwa adimu kwa hapo awali na kufanya bidhaa zote muhimu zinamfikia mwananchi wa kawaida popote pale nchini.

Ni kwa njia hii alijizolea umaarufu kwa wananchi wake ambapo ilifikia kipindi tukamjua kwa jina maarufu kuwa “Mzee Ruksa” ikimaanisha kuwa kila kitu ilikuwa ni ruhusa kukitumia utakavyo ili mradi tu usivunje sheria!.

Katika hali wengi walilalamika kuwa uchumi wa nchi ulishuka, hasa thamani ya pesa ilikuwa chini, hali ambayo ilifanya kijana wa kawaida asiyefanya kazi kuwa na pesa nyingi ambazo zilisababisha mfumko wa bei kuwa katika kiwango cha juu zaidi.

Hakuishia hapo tu bali alihakikisha kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao unaunda Tanzania unadumu na kuendelea kuwepo katika ramani ya Dunia na kufanya nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi chache zilizoweza kudumu katika muungano wa nchi mbili katika muda mrefu.

Baada kumaliza ngwe yake ya miaka 10 kama katiba yetu inavyoonyesha na kuruhusu kuongoza, alimwachia tena rais wa awamu ya tatu Ndugu Benjamin William Mkapa usukani wa kuiongoza Tanzania yetu ikiwa katika hali ya utulivu na amani.

Pia kitu cha muhimu zaidi ambacho kiliweza kufanyika chini ya rais huyu wa awamu ya tatu ni hali ambayo nchi yetu iliweza kubadilisha historia yake na kuingia katika mfumo wa vyama vingi kutoka kwenye mfumo wa chama kimoja.

Pamoja na kuwa wananchi wengi hawakuwa tayari kupokea mfumo huo kwa kudhani kuwa ilikuwa ni sababu ambayo ingeweza kusababisha machafuko nchini na kupoteza utulivu tuliokuwa nao, lakini kwa busara za kiongozi huyu pamoja na muasisi wa Taifa hili Mwalimu Nyerere walishawishi ngazi husika na hatimaye vyama vingi nchini vikaruhusiwa.

Baada ya hapo rais wa awamu ya tatu Ndugu Benjamin William Mkapa, alichukua uongozi wa nchi akiwa rais wa kwanza Tanzania chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.

Kazi kubwa aliyokuwa nayo ilikuwa ni pamoja na kufufua uchumi wa nchi yetu ambao ulionekana kulegalega na kuhakikisha kuwa mfumo wa bei na hali za kimaisha kwa watanzania zinaboreshwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa miundo mbinu yote muhimu inaundwa.

Ni ukweli mtupu kama mimi ningekuwa na uwezo wa kubadili katiba ili Mr. Ben aweze kuongoza tena katika kipindi kingine cha miaka hata 20 ningefanya hivyo ili tu kuhakikisha kuwa anabaki madarakani na kuendeleza mipango yake ya baadae.

Lakini nina kila sababu za kumpongeza rais wetu mpendwa kwa kuthamini na kujali katiba ya nchi kama inavyoeleza kuwa kiongozi wa ngazi ya juu serikalini kama rais ataweza kukaa madarakani kwa vipindi viwili vya uongozi tu ikimaanisha miaka kumi tu.

Katika hili amejali na kufanya hvyo licha ya wadau mbalimbali wa duru za kisiasa kumuomba na kumshauri kuwa aweze kubadilisha katika na hatimaye kuongoza, kwa nampongeza sana “HONGERA SANA MR. BEN” kwa kufuatilia katiba ya nchi, hii inaonyesha ni kiasi gani umekomaa kisiasa na kutokuwa na tamaa ya madaraka.

Dunia nzima ukimtaja Benjamin Mkapa wanamfahamu kama enzi hizo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alivyosifika kwa ujasili wa kutokuona haya kusema ukweli, naye raisMkapa amesifika kuwa ni kiongozi shupavu na mwenye uwezo wa kuongoza bila kutetereka.

Kwa hili tuna kila sababu ya kumshukuru mungu kwa kutujalia viongozi wenye uwezo wa kuongoza nchi vizuri, hasa hasa kuhakikisha kuwa usalama na umoja wa nchi yetu unaendelea kudumu na kutuelekeza vyema ili kuyafikia hayo maendeleo endelevu katika karne hii ya sayansi na teknolojia.

Hapa nimejaribu kugusia japo kwa kidogo tu uongozi wa awamu zote tatu kuanzia uhuru hadi sasa chini ya rais Mkapa, ambapo kumekuwa na tofauti kubwa sana ya kimaendeleo toka nchi yetu ipate uhuru enzi hizo tukinunua sabuni kwa kupanga Mstari hadi sasa tukinunua sabuni kwa kuletewa mlangoni, raha iliyoje!.

Pamoja na hayo mwaka huu tupo katika vuguvugu jingine la kumtafuta kuiongozi wa nchi yetu katika uchaguzi mkuu baadae mwaka huu ambapo tunategemea kuwa kiongozi tutakaye mpata basi aendeleze mazuri yote yaliyoanzishwa na viongozi hawa waliomtangulia.

Tunapofikia hapa, tena swali moja ambalo hunisumbua sana kichwani kama hpo mwanzo nilianza kwa kusema kuwa ni kitendawili au ni swali la kutumia kikokotozi ili kuweza kulijibu, hali ambayo huwa sipati njia sahihi ya kupata jibu hilo.

Historia inaonyesha kuwa katika Tanzania viongozi wote walioiongoza nchi hii wametoka katika makabila madogo tu ambayo hayana majina makubwa kulinganisha na makabila mengine nchini ambayo yana nguvu na uwezo mkubwa.

Swali langu haliishii hapo, je nini athari za viongozi kutoka kwenye makabila madogo katika uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu? Je historia itajirudia tena?.

Hili swali hunisumbua sana ndio maana nimeamua kuliandikia makala haya, kuwa historia inaonyesha kuwa viongozi wote wa ngazi ya juu waliowahi kuiongoza nchi yetu wametoka katika makabila madogo sana hapa nchini na je nini athari zake kwa uchaguzi wa mwaka huu.

Hapa hatuzungumzii ukabila kama wa Rwanda na Burundi au Wahutu na Watsi ambao kila wanapokutuna ujue kuwa hapo shughuli ipo ni kuwahiana tu na kumalizana ama kwa mapanga au silaha zozote zinazoweza kupatikana katika eneo hilo.

Bali ukweli ni kwamba tunajadili majaaliwa ya nchi yetu hapo baadae, huku tukikumbuka kuwa nchi yetu haina Dini wala Kabila maalumu bali watu wake wana makabila yao na dini zao hili hata mwalimu mwenyewe enzi za kuijenga nchi yetu alilikemea kwa nguvu zote na hili halina mjadala ndio maana nimepata jeuri ya kulijadili hili.

Tuchukue kuwa mwalimu Nyerere alitoka katika kabila dogo sana linaloitwa kabila la Wazanaki kutoka katika mkoa wa Mara, ni kabila dogo sana ambalo lilitoa kiongozi shupavu sana na wakuheshimika duniani kote.

Pia rais Mwinyi alitoka katika kabila dogo tu huko Zanzibar, ambaye naye aliweza kufanya yaleyale ya kuiongoza nchi katika misingio sahihi na safi ambayo iliifikisha nchi katika hatua hiyo iliyoendelezwa na Ndugu Mkapa.

Ukija kwa ndugu yangu ambaye mimi hupenda kumwita Mr. Ben, yeye naye katoka huko kusini kwenye kabila moja dogo tu la Mmakonde, pia naye kama wenzake amefanya maajabu na kuingoza Tanzania kwa staili yake hali iliyofanya kila mtu kumlilia yeye.

Hapa nimelenga kuuliza umma kuwa je yale yaliyotokea hapo awali ya kuwa na viongozi bora kutoka kwenye makabila madogo yasiyo na majina yataendelea tena kutoa viongozi wa kundi hilo hilo au itakuwa tofauti kwa mwaka huu?.

Kwa njia moja ama nyingine nchi yetu inahitaji kiongozi aliyeshupavu mwenye uwezo wa kiutendaji anayeweza kuwajibika kwa watu wake kwa muda wake wote atakao kuwa madarakani ili kuhakikisha kuwa anafanya yaliyomema.

Kama kiongozi mmoja anayewania uongozi huo alivyosema kuwa Tanzania haijawa maabara ya kujaribia viongozi na hapa tujue kuwa kabila haina maana ya kuwa ndio kigezo cha kutoa kiongozi bora bali ni uwezo wa mtu binafsi ndio utakao amuru ni nani anaweza kufanya vizuri.

Vilevile misingi ya uongozi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere toka anadai uhuru wa nchi yetu ndio itumike kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendeleza uongozi mzuri na kuhakikisha kuwa amani inaendelea kudumu.

Hivyo basi hili swali siku zote huwa linaumiza kichwa changu katika kinyang’anyiro cha kuwania urais miongoni mwa wagombea waliojitokeza kuchukua fomu za kuomba lidhaa ya wanachama wa vyama vyao ili waweze kugombea urais kupitia vyama vyao.

Kwa njia moja ama nyingine jibu la swali hili litakuwa wazi baada ya vyama kuteuwa wagombea wao wenye uwezo wa kuongoza umma wa watanzania pasipo kujali Kabila , dini wala ukanda kwani nchi yetu inaendeshwa kwa njia za kidemokrasia na demokrasia hiyohiyo ndiyo itakaye amua kuwa nani anafaa pasipo kumuangalia usoni au kabila lake.

Hivyo basi ni nafasi ya vyombo husika kama Halmashauri kuu ya CCM na vyama vingine kuhakikisha kuwa vinateuwa viongozi safi wasio na mawaa ambao watafuata nyao za viongozi waliopita na kutuletea mafanikio mazuri.

Elimu, uwezo wa kuongoza, jitihada binafsi, kutokuwa na ubinafsi, kuwajali walio chini na kutumia muda mwingi kuwatumikia wananchi ni mojawapo ya sifa ambazo rais ajaye anatakiwa kuwa nazo na si sifa ya ukabila, udini na ukanda, Mungu ibariki Tanzania ipate kiongozi mwenye kujali wananchi wake!.

2 Comments:

  • At 5:21 PM GMT+3, Blogger ARUPA said…

    E bwana unatesa kishenzi na akaunti yako

     
  • At 2:57 PM GMT+3, Anonymous Anonymous said…

    Avoid verbosity.

    Don't praise Mkapa that is none of your business

     

Post a Comment

<< Home