"Kupanga ni Kuchagua"

Kila mwanadamu ana mamlaka ya kubadilisha maisha yake kwa kutumia mazingira aliyo nayo! Mipango mibovu ya maisha yake husababisha maisha yake kuwa mabovu na Mipango bora ya maisha yake husababisha maisha yake kuwa Bora. Hivyo basi chagua maisha yako unataka yaweje?

Saturday, September 10, 2005

Mzee wa Kiraracha hatuendi hivyo.

Ni muda sasa toka pazia la kampeni kufunguliwa na kuruhusu wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika vyama vya siasa nchini kunadi sera zao kwa wananchi kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 30 mwaka huu.

Ni katika kipindi hiki ambapo tumeshuhudia wagombea wakijitokeza majukwaani wakijinadi kwa wananchi, kila mmoja akijitahidi kuainisha sababu zinazomfanya awaombe wananchi kumpa nafasi ya kumchagua ili awe kiongozi wao katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Zoezi hilo pia limekuwa likienda sanjari na kuvinadi vyama vyao kupitia sera za vyama husika huku wagombea hao wakijitahidi kuainisha kile kilichoko ndani ya ilani au sera za vyama vyao, ambazo kwa ujumla zimelenga katika kumkwamua Mtanzania bila kujali kuwa ni kwa namna gani

Kwa kifupi ni kuwa, kipindi hiki ni muhimu sana kwa walio na hata wale wasiokuwa wanasiasa kwa ujumla, kwasababu pande hizo zote zinategemeana katika kufanikisha mchakato huu kwa ujumla wake.

Ni sawa na kipindi cha kukaribia msimu wa kilimo ambacho wakulima hukitumia kusafisha mashamba yao tayari kwa kupanda mbegu mvua zikianza.Kipindi hiki kinatumika kwa wanasiasa kuweka wazi mikakati yao ya baadae kwa wapiga kura wao ili waweze kuwachagua.

Umuhimu wa kipindi hiki hauishii hapo tu kwani kwa upande wa wananchi hutarajia kujulishwa kwa kina wapi tulipokwama, kwanini tumekwama na kuainishiwa ni nani, kwanini na kwa namna gani atawaongoza kujikomboa kutoka katika lindi la umasikini.

Kwa bahati mbaya katika kampeni hizi kunajitokeza vitendo visivyo vya kistarabu kwa wapiga debe au viongozi wa vyama husika katika nafasi mbalimbali, kukitumia kipindi hiki kwa kuchafua majina ya wengine badala ya kuweka wazi sera zao.

Katika ufuatiliaji wangu wa kampeni hizo toka zilipozinduliwa rasmi na Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC), kuna baadhi ya wagombea na vyama vyao ambao hawajawahi kupanda jukwaani na kutangaza sera zao au za vyama vyao na badala yake kuona wamepata ulingo wa kuikashfu serikali na wagombea wa chama tawala.

Ni vyema ikafahamika kuwa Watanzania wa sasa sio wale tuliokuwa tunawafahamu katika miaka ya sabini na themanini. Watanzania waliokuwa wakiishi kwa utamaduni wa "ndio mzee", ambao walikuwa hawana uwezo wa kuhoji jambo ila kukubaliana nalo kwa vile limetolewa na kiongozi wa ngazi ya juu pasipo kujali baya au zuri.

Si lengo langu kuelezea kila jambo na kwa kila chama bali nataka kuangalia mwenendo mzima wa kampeni kupitia chama cha TLP maarufu kama "Jogoo", kinachoongozwa na "Mtaalamu wa mabomu au mzee wa Kiraracha", Augustine Mrema, ambazo zilianzia mkoani Mwanza.

Kwa mfuatiliaji mzuri wa kampeni atakubaliana nami kuwa, Mheshimiwa huyu toka alipozindua kampeni zake hajawahi kupanda jukwaani na kunadi sera kwa mantiki halisi ya sera zenye mrengo wa kumkwamua Mtanzania, kuwa anatarajia kufanya nini kwa wananchi endapo atachaguliwa kuiongoza nchi, kama ipo basi ilikuwa ni kibwagizo tu baada ya kumaliza kuiponda serikali na Chama cha Mapinduzi na viongozi wake.

Hili liko wazi na halina ubishi na kwa wananchi alimopita Mrema wataniunga mkoni kuwa kila anapopanda jukwaani husikika akikipaka matope Chama cha Mapinduzi na mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho Jakaya Kikwete kuwa ni wabadhirifu wala rushwa, wasiojali wananchi wake, hawafai kupewa uongozi na mambo mengineyo ili mradi nafsi yake iridhike kuwa amekiponda chama hicho vya kutosha.

Pia amesikika kila mkutano anaohutubia akiwanyooshea vidole vingozi wa dini wakiwemo maaskofu kuwa wao ndio watakao changia kushindwa kwake eti tu kwa sababu baadhi yao walikwisha sema 'Kikwete ni Chaguo la Mungu'.

Wananchi wengi husikika wakicheka na kushangilia anapohutubia haya, si dhani kama wananchi wanakuwa wameridhika na maneno yake au wanashangilia tu kuwa Mheshimiwa Mrema ni mtaalamu wa kusema porojo na wanajua kuwa hana sera.

Mara kwa mara amesikika akisema kuwa Kikwete si Kijana ni mzee ila sura yake inasaidiwa na mkorogo tu, hili nalo hunifanya nicheke na hatimaye mbavu zangu kuuma, kwani sera ya Mrema ni ukijana au uzee? na uzee wa Kikwete yeye unamuathiri nini?.

Haya ni maswali ambayo hujiuliza kila mara na kukosa jibu la uhakika kwani kwa mwananchi wa kawaida anayetoka nyumbani kwake kwenda kwenye mkutano wa hadhara tena wa Rais mtarajiwa hatarajii mtu huyo kuanza kumzungumzia mpinzani wake eti kuwa ni mzee kwani yeye hajui hayo!.

Nafikiri msemo mmoja wa zamani umempitia kando mheshimiwa huyu kuwa "Usiuze ng'ombe wako kwa kumponda wa mwenzio" kama yeye kaamua kuingia kwenye biashara hii basi aiuze kwa kutaja sifa za bidhaa yake na si kuiponda bidhaa ya CCM ambayo tayari iko sokoni.


Kwa njia moja ama nyingine atakuwa (bila yeye kujijua) anakijenga Chama cha Mapinduzi na kukipa sifa kubwa kwa wananchi kwani kukiponda tu bila kueleza sera zake ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwani wananchi hawatajua waende wapi na itawabidi wabaki walipo CCM kwani wewe huweki wazi sera zako watakuchaguaje? wakati huna sera unazozitangaza kwao?.

Mtu au mgombea wa aina hii hutoa nafasi kwa wananchi kumtilia mashaka kuwa hata wakimchagua ataongozaje nchi wakati hana sera na kama anazo haziweki wazi kwa wananchi ili waziweke kwenye mizani na kupima uzito ni zipi zinafaa kati ya za chama chake na vyama vingine.

Ikumbuke kuwa viongozi wa dini ni watu muhimu sana katika kuleta amani katika nchi yetu na kama kwa sasa hana uhusiano nao na anawalaani kila mkoa anaopita itakuwaje kama atachaguliwa kuliongoza dola, si viongozi hawa watakuwa hatarini.

Mimi naamini kuwa maaskofu na viongozi wa dini hao ni miongoni mwa raia wa Tanzania hivyo wanayo haki ya kusema katika jamii jambo ambalo wanafikiria katika vichwa vyao ndio maana walisema kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu kama wazo binafsi na lisilo wahusisha watu wengine au dini zao.

Kwa wafuatiliaji wa taarifa mbalimbali za vyombo vya habari, sidhani kama kuna mtu anayeweza kukubaliana na ukweli kuwa viongozi hao walifanya makosa kama anavyotaka kutuaminisha mgombea huyu, kwasababu hakuna hata sehemu moja ambako viongozi hao walisema kuwa misimamo yao ni misimamo ya waumini wao.

Hivyo isiwe sababu kuwa kwa vile baadhi ya viongozi hao walisema kuwa Kikwete ni chaguo la mungu basi ndio kweli limekuwa chaguo la Mungu ila chaguo hilo litajulikana hapo Oktoba 30 baada ya uchaguzi mkuu kufanyika ndipo tutajua chaguo la Mungu ni lipi.

Kwa hali hii naweza kusema kuwa ni kufilisika kimawazo, Mtazamo, sera na malengo ya hapo baadae kwa kiongozi mkubwa kama Mrema kwani haifai kupoteza muda wa wapiga kura wanaojitokeza kuja kukusikiliza kwenye mikutano yako badala yake hawapati kitu walichofuata (sera) na kupata kashfa zinazoelekezwa CCM.

Nakumbuka siku moja nilipohudhuria mkutano mmoja wa kampeni wa Mrema katika eneo la Mvumi misheni hivi karibuni mkoani Dodoma alipoanza kuhutubia na wananchi kumsikiliza walichoshwa na kashfa hizo na mmoja wao alipayuka na kusema "tunataka sera! na sio majungu".

Kwa hali ya kawaida hapo awali katika miaka niliyoitaja huko nyuma sikutegemea mwananchi katika eneo kama hilo kuuliza kitu kama hicho ila imefika kipindi ambacho wananchi wanahitaji kiongozi mwenye mitazamo inayoridhisha na malengo mazuri katika kuhakikisha kuwa maisha yao yanaboreka.

Hiyo inathibitisha kuwa wananchi wa sasa sio wa "Ndio mzee" bali ni wananchi ambao wanataka kujua kuwa utakapoingia madarakani utashirikiana nao vipi na utawafanyia nini sio wao watakufanyia nini na hasa wanachojali ni sera zenye kuleta maendeleo.

Hapa napenda kushauri kuwa kama ndio mwenendo mzima wa kampeni za Chama Cha TLP zitakuwa namna hii bila kuwa na mabadiliko ya kuanza kutangaza sera yake ni heri fedha zinazogharamia kampeni zitumike kwa njia nyingine kwani kampeni bila kunadi sera ni sawa kuwaibia Watanzania.

Ikumbukwe kuwa fedha za kampeni ambazo vyama mbalimbali vinavyoshiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, sio fedha kutoka kwa wahisani bali ni fedha zilizopatikana kutokana na kodi za Watanzania hao hao ambao mnawadanganya na ambao wanauchungu na kodi zao kwasababu hawaoni kama zinawanufaisha.

Vipo vyama vingi ambavyo vinafanya kampeni za 'Kugombania' badala ya kugombea kuingia Ikulu kwa kutokuwaeleza wananchi malengo yao bila kujua kuwa muda ni mfupi sana kama utatumiwa visivyo na ni mrefu sana kama utapangiliwa kwa njia nzuri kwa hiyo staili hii ya kampeni haifai na itafanya mpaka muda unakwisha wananchi ambao ndio walengwa hawajajua kuwa sera ya TLP na mgombea wake Mrema iko vipi.

Naamini kuwa chama cha TLP na mwenyekiti wake Augustine Mrema mna sera ya kutosha tena mpya kama Digrii yako iliyokuja kwa Faksi hivi karibuni tu ikimaanisha kuwa hata vumbi haijapata, hivyo muda huu ndio wa kunadi sera hizo na usitegemee kusoma magazeti ili kupata ushahidi wa kuiponda CCM na viongozi wake.

Pia acha kuwalaumu na kuwalaani viongozi wa dini kwani hata wao wanaweza kukulaani, badala yake wafikishie wananchi ujumbe wa chama chako katika mikutano unayoihutubia ili wajue kuwa umelenga nini katika miaka mitano ijayo.

Mzee wa Kiraracha tunataka sera zilizokufanya upande jukwaani kutuhutubia au wewe unapenda kupanda jukwaani na kuwatukana viongozi wa serikali kwa kuwatolea maneno ya kebehi wenzio haoo wanakata mbuga, na jua kuwa usije kumbuka shuka wakati kumekucha!

1 Comments:

  • At 2:58 PM GMT+3, Blogger Rama Msangi said…

    Ni kweli na ni safi ila ulikosa picha ya mzee wa Kiraracha? yaani unakosa picha ya mzee wa NJI

     

Post a Comment

<< Home