"Kupanga ni Kuchagua"

Kila mwanadamu ana mamlaka ya kubadilisha maisha yake kwa kutumia mazingira aliyo nayo! Mipango mibovu ya maisha yake husababisha maisha yake kuwa mabovu na Mipango bora ya maisha yake husababisha maisha yake kuwa Bora. Hivyo basi chagua maisha yako unataka yaweje?

Saturday, October 15, 2005

Mkapa anayo nafasi ya kuwapa HakiElimu kujirekebisha

HIVI karibuni Rais Benjamin Mkapa, alipiga marufuku Taasisi ya HakiElimu kujishughukisha na masuala ya elimu katika kipindi cha siku 30 zilizosalia za uongozi wake, huku akiisukumizia lawama lukuki kuwa ni wapotoshaji wa maendelea ya sekta ya elimu nchini.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Ikulu ndogo ya Chamwino, mjini hapa, ulioandaliwa na wanakijiji kwa ajili ya kumuaga, Rais Mkapa, alisema taasisi hiyo imekuwa ikipotosha ukweli halisi wa hali ya elimu nchini na kuwashushia hadhi watendaji wake wakiwemo walimu.

Alisema hataki katika uongozi wake kusikia taasisi hiyo ikijihusisha na jambo lolote linalohusiana na elimu katika shule za hapa nchini na kuachia dhamana na majaliwa ya asasi hiyo mikononi mwa Rais wa awamu ya nne.

Alisema Hakielimu wamekuwa wakipotosha elimu ya Tanzania kwa kutoa matangazo ambayo kwa njia moja au nyingine yalikuwa yanawajengea wananchi hali ya kudai haki bila wajibu.
"Nasema katika uongozi wangu sitaki kusikia HakiElimu wanakanyaga katika shule zetu, ni wapotoshaji na ni ujinga kuwaruhusu watu kama hao," alisisitiza Rais Mkapa.

Alisema hata vumilia hata siku moja kuona ujinga huo ukiendelea katika nchi yake ambayo amepewa mamlaka na wananchi kuiongoza na kwamba hatua hiyo itaendelea hadi pale taasisi hiyo itakapo elimika na kuacha upotoshaji huo, na kuifanya Serikali kuangalia upya msimamo wake.

Alisema hata wafadhili wanaoifadhili taasisi hiyo, wanatafuta uwezekano wa kuboresha elimu yao huko kwao na kufikia kiwango kizuri na kuhoji kwanini wadharau juhudi za kuinua elimu zinazofanywa na Serikali ya Tanzania.

Alitumia nafasi hiyo kumpongeza Waziri wa Elimu na Utamaduni, Bw. Joseph Mungai kwa uamuzi wake wa kuipiga marufuku taasisi hiyo na kusema kuwa ni hatua sahihi. Hatua hiyo ya Rais Mkapa, imekuja baada ya asasi hiyo kulalamikiwa na Serikali kuhusu matangazo yake inayoyatoa katika vyombo vya habari kulenga kuipinga Serikali katika juhudi zake za kuiboresha elimu nchini.

Rais Mkapa pamoja na kuzungumzia mambo mengi kuhusiana na asasi hiyo alimtaka Waziri wa Elimu na Utamaduni, Bw. Joseph Mungai, kutobabaika katika uamuzi wake kwani imeonesha ni kiongozi shupavu na anayefaa.

Pamoja na kusema hivyo aliacha majaliwa ya asasi hiyo kwa Rais ajaye kama ataona mabadiliko yoyote ya kiutendaji katika asasi hiyo na kufikiria uamuzi wa kuirudisha tena kufanya kazi kwa mujibu wa taratibu za nchi.

Ninavyojua mimi kiongozi wa nchi akibariki jambo ndio uamuzi wa mwisho au ni amri, amri hiyo ilianzia kwa Wizara ya Elimu na Utamaduni na baadaye baadhi ya wananchi walisikika wakilalamika hatua hiyo na kuitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kuiruhusu asasi hiyo kuendelea na kazi zake kama kawaida kabla ya sasa Rais Mkapa kubariki uamuzi wa Bw. Mungai.

Kutokana na agizo hilo bila shaka sasa asasi hiyo ya HakiElimu haitafanyi kazi tena kwa mujibu wa amri iliyotolewa na Rais Mkapa, katika kukanyaga katika shule mbalimbali nchini, ingawa bado wanaweza kuendelea na kazi zao za kawaida.

Uamuzi wa Rais Mkapa, huenda kwa njia moja au nyingine, ukawa uamuzi sahihi wenye lengo la kutetea maslahi ya nchi ambayo yanahakikisha kuwa taratibu za ndani ya nchi hazivunjwi na AZISE zilizoanzishwa nchini kwa lengo la kukuza maendeleo ya sekta mbali mbali.

HakiElimu pamoja na kuandaa na kutoa machapisho ambayo yalikuwa yanaipinga Serikali katika juhudi zake za kuendeleza elimu hapa nchini, ilifanya baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yanaeleza hali halisi ya mazingira ya elimu nchini.

Katika baadhi ya mambo ambayo HakiElimu ilikuwa inafanya vizuri ni pamoja na kuonesha jinsi watoto walemavu walivyokuwa wanakosa haki zao kwa kuchanganywa na watoto wasio walemavu katika masomo yao.

HakiElimu kwa upande mwingine walijitahidi kuonesha ni jinsi gani pesa za MMEM zilivyokuwa zikiliwa na wafanyakazi wa ngazi ya juu katika Halmashauri za Wilaya kwa kuwaelekeza walimu sehemu za kununua vifaa vya shule.

Pia asasi hiyo ilikuwa inawasaidi wananchi kuibua hisia za kujua haki yao katika uendeshaji wa shule zilizopo katika maeneo yao ikiwa ni pamoja kujua mambo muhimu kama mapato na matumizi ya shule na taarifa muhimu.

Kwa upande mwingine asasi hiyo ilijaribu kuweka wazi baadhi ya kero za wanafunzi katika masomo yao kwa mfano, Serikali kudai kuwa haiwabagui watoto wenye walemavu na wasio na ulemavu wakati shule zinazojengwa zina ngazi ndefu ambazo zinawawia vigumu wanafunzi walemavu kuingia madarasani.

Yote haya yalikuwa mema ya asasi hiyo na mengine mengi ambayo yalifanywa katika mlolongo huo na ambayo sio rahisi kuyataja yote ili mradi kufikisha ujumbe kwa Watanzania kuhusiana na kero mbalimbali katika sekta ya elimu.

Lakini basi sidiriki kubeza uamuzi uliotolewa na mkuu wa nchi, juu ya asasi hiyo na naamini kuwa, amefikiria kwa makini, amepitia vigezo mbalimbali na kuamua kutoa uamuzi kama huo.

Nadhani mantiki ya Rais Mkapa ni kwamba asasi hiyo imekuwa pinzani kwa kila jambo linalofanywa na Serikali katika harakati zake za kuboresha elimu, pasipo walau siku moja kutamka kuwa kuna jambo katika elimu ambalo limewafurahisha au limefikia kiwango kizuri na cha kupongezwa.

HakiElimu pia ilitoa machapisho mbalimbali ya utafiti ambayo yalikuwa yanaipinga Serikali katika ukuzaji wa sekta ya elimu, machapisho hayo yalikuwa yanasambazwa mashuleni na yalikuwa yanawavunja moyo walimu pia kuwashushia hadhi zao katika juhudi za ufundishaji.
Kama alivyozungumza Rais Mkapa, wakati akitoa agizo hilo, alisema baadhi ya matangazo yake yalilenga kuwajengea tabia Watanzania ya kudai haki tu bila kuwajibika.

Kwa mujibu wa Rais Mkapa, si rahisi kupata haki bila kuwajibika, bali kinachotakiwa ni wajibu kwanza halafu haki inafuata, na pengine Serikali imebaini kwamba ungefikia wakati ambao wananchi wangepinga kila jambo linalofanywa na Serikali kuhusu elimu.

Pamoja na mambo hayo, bado HakiElimu wanao muda wa kufikiria na kujirekebisha pale walipokuwa wanakosea kwani kwa mujibu wa Rais Mkapa, Serikali itafikiria upya uamuzi wake pindi asasi hiyo itakapojirekebisha.

Katika hali halisi, Serikali ya awamu ya nne ambayo imebakiza kama mwezi mmoja tu kuingia madarakani, inaweza kufikiria kuiruhusu asasi hiyo kuendelea na uhusiano na ushirikiano na shule za nchini, kama itajirekebisha katika mambo ambayo yamesababisha kuzua mgogoro na Serikali.

HakiElimu isikate tamaa, kwa sasa ikae chini na kuangalia ni mambo gani ambayo walikuwa wanakwenda kinyume na taratibu za Serikali, na baada ya kuyarekebisha waombe tena nafasi ili waweze kuendelea na kazi zao kama kawaida.

Tunaihitaji sana HakiElimu katika kuikosoa Serikali kwenye mambo ambayo inakwenda kinyume na Sera zake, lakini hatua hii ichukuliwe kama changamoto ya kudumisha na kukuza ushirikiano baina yake na Serikali, lengo likiwa ni kukuza kiwango cha elimu nchini.

Kukosolewa ni jambo la kawaida katika jamii, hivyo HakiElimu wachukulie agizo hilo la Serikali kama chachu ya kutumia nafasi hiyo kujadili na kurekebisha makosa yaliyopo ili kufufua umpya ushirikiano baina yake na Serikali.

10 Comments:

Post a Comment

<< Home